Story by Our Correspondents
Mgombea wa kiti cha ugavana katika kaunti ya Kilifi kupitia chama cha ODM Gedion Mung’aro amemteua Margaret Mbetsa Chibule kuwa mgombea mwenza wake katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika halfa iliyoandaliwa katika uwanja wa Mkwajuni mjini Kilifi, Mung’aro amesema huu ni wakati mwafaka wa kutambua juhudi za wanawake katika siasa kwani wamechangia pakubwa kufanikisha maendeleo nchini.
Mung’aro hata hivyo ameahidi kuhakikisha anakabiliana kikamilifu na swala la ufisadi, kuboresha muundo msingi, kubuni ajira kwa vijana sawa na kuwatambua akina mama na wale wanaoishi na uwezo maalum ili kubadili sura ya Kilifi kimaendeleo.
Kwa upande wake Mgombea mwenza wa Mung’aro, Margaret Chibule ameahidi kushirikiana na Mung’aro katika kufanikisha maendeleo huku akisema swala la elimu katika kaunti hiyo litapigwa jeki zaidi sawa na kupatikana kwa maji safi na afya bora.
Naye Mbunge wa Ganze ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Kilifi Tedy Mwambire, amesema ugatuzi umechangia maendeleo mengi mashinani huku akihoji kwamba serikali itakayobuniwa na Mung’aro itaboresha zaidi maendeleo.
Hata hivyo Seneta wa kaunti hiyo Stewarts Madzayo amempiga debe Mung’aro kuchanguliwa kama gavana wa kaunti hiyo, ikisema wakati wa uongozi wake kama Katibu mkuu msimamizi katika Wizara ya Ugatuzi na Ardhi alichapa kazi.