Story by: Charo Banda
Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amefika mbele ya Mahakama kuu ya Malindi kutoa ushahidi wake kwenye kesi ya kupinga ushindi wake kama gavana iliyowasilishwa Mahakamani.
Kesi hiyo ambayo iliwasilishwa na wapiga kura watatu akiwemo, Justice Chinga Chirume, Justin Charo Baya na Salim Chai Tsui, waliishtaki Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC na gavana Mung’aro kwa madai ya kutoandaa uchaguzi uhuru, haki na uwazi.
Akiwa mbele ya Jaji wa Mahakama hiyo Anne Adwera Onginjo, Gavana Mung’aro ameeleza jinsi alivyoshiriki uchaguzi huo huku akiweka wazi kwamba uchaguzi huo ulizingatia kanuni zote zilizohitajika kulingana na jinsi alivyoshuhudia
Hata hivyo mapema siku ya Alhamis Mshirikishi mkuu wa Tume ya IEBC kaunti ya Kilifi Hussein Gurre, alifika mbele ya Mahakama hiyo kuu ya Malindi na kutoa ushaHidi wake kuhusiana na kesi hiyo ambapo walalamishi wanadai kwamba uchaguzi wa ugavana kaunti ya Kilifi ulishuhudia udanganyifu.
Wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo wa Agosti 9 mwaka wa 2022, Gavana Mung’aro wa chama cha ODM alipata jumla ya kura 143,773, Aisha Jumwa wa chama cha UDA akapata kura 68,894 na George Kithi wa chama cha PAA akapata kura 64,326.