Story by Gabriel Mwaganjoni–
Mrengo wa kisiasa wa Kenya Kwanza umezidi kuushambulia ule wa Azimio la Umoja ambao umedai kuishinikiza Serikali kupunguza bei ya unga wa Mahindi kutoka shilingi 230 hadi shilingi 100 pekee.
Mmoja wa Vinara wa mrengo huo ambaye pia ni Kinara wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi ameitaja mbinu hiyo kama uongo wa kisiasa unaolenga kumhadaa mkenya huku akiwataka wananchi kuwa makini.
Akizungumza katika kampeni za kisiasa za mrengo wa Kenya Kwanza magharibi mwa Kenya, Mudavadi ameitaja kauli hiyo ya Serikali kama uongo na usiyostahili kwa mkenya aliyechoshwa na uongozi duni na kupanda kwa gharama ya maisha.
Wakati uo huo amemkosoa Rais Kenyatta kwa kushindwa kuboresha sekta ya kilimo nchini na badala yake kutumia mbinu za kuwahadaa wakenya licha ya wananchi kuhangaishwa na gharama ya maisha.