Maafisa wa polisi eneo la Kisauni kaunti ya Mombasa wamempiga risasi na kumuua mshukiwa mmoja wa uvamizi uliofanyika usiku wa kuamkia leo katika eneo la Mshomoroni, na kuwawacha wanafunzi wawili wa chuo Kikuu cha TUM na majeraha mabaya.
Kamanda mkuu wa polisi eneo la Kisauni Julius Kiragu, amesema walifahamishwa kuhusu uvamizi huo na kufika eneo hilo mara moja na kupambana na majambazi hao waliokuwa wamejihami kwa visu na mapanga.
Kulingana na Kiragu, polisi wamenasa mapanga matatu na kisu kimoja kirefu aina ya Machete kutoka kwa vijana hao huku wakiimarisha msako mkali dhidi ya genge hilo.
Hata hivyo Wanafunzi hao wawili waliyokatwa mapanga kichwani, mikononi na mabegani wanapokea matibabu ya dharura katika hospitali kuu ya rufaa kanda ya Pwani.