Mtu moja amefariki huku mwengine akiwa hajulikani aliko baada ya boti walilokuwa wakisafiria kuzama katika eneo la Mkupe huko Miritini Kaunti ya Mombasa usiku wa kuamkia leo.
Kulingana na Maafisa wa polisi eneo la Changamwe Joseph Kavoo, boti hilo lilikuwa limewabeba wafanyikazi kumi wanaoendeleza ujenzi wa daraja eneo la mradi wa dongo kundu katika eneo hilo la Mkupe.
Japo watu 10 wameokolewa katika mkasa huo, mmoja amefariki na mwili wake umepatikana mapema leo ukielea katika mkono wa Bahari hindi eneo hilo la Mkupe huku mmoja akiwa bado hajulikani aliko.
Juhudi za kumsaka mwanamume huyo zinaendelea kwa sasa huku wapiga mbizi kutoka Serikali ya Kaunti ya Mombasa, wale wa Shirika la Msalaba mwekundu, Mamlaka ya ubaharia nchini na jeshi la majini wakiimarisha msako wao ili kumnusuru mwanamume huyo.
Mwili wa mwanamume uliyopatikana umepelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu Kanda ya Pwani, huku polisi wakisema boti hilo limeshindwa kustahimili mawimbi ndiposa likapinduka baharini.