Mtangazaji wa kituo cha radio cha Radio Kaya Beatrice Dama Kahindi ametunukiwa tuzo ya “Balozi wa Amani na Utamaduni” na muungano wa utamaduni wa wilaya ya Malindi (MADCA).
Dama alitunukiwa tuzo hiyo katika sherehe za kumkumbuka shujaa Mekatilili wa Menza zilizofanyika huko Shaka Hola, Kaunti ya Kilifi.
” Ni furaha kuweza kutunukiwa tuzo hii lakini pia ni changamoto kubwa kwangu kuona kuwa nazidi kuulinda utamaduni wetu,” amesema Dama.
Kando na mtangazaji huyo, mtetezi wa haki za watoto Mvera Kazungu na Mjumbe mteule Beatrice Jave Mbuche pia walitunukiwa tuzo hiyo.
Mvera ambaye ni muasisi wa shirika la kijamii la Fimbo Initiative aliweza kutuzwa kutokana na juhudi zake za kupambana na madhila yanayofanyiwa watoto na vilevile kuvalia vazi la kitamaduni alipozuru nchi ya Marekani.
“Utamaduni wetu ni wa kujivunia na unapojihusisha na utamaduni sio kupitwa na wakati. Tukizidi kudumisha utamaduni wetu hatutakuwa na mmomonyoko wa madili kama tunavyoshuhudia sasa,” amesema Mvera.
Mekatilili wa Menza ni shujaa aliyeiongoza jamii ya Wamijikenda dhidi ya utawala wa mkoloni nchini Kenya.
Taarifa na Dominick Mwambui.