Msukosuko wa kiusalama umetajwa kuanza kushuhudiwa katika kaunti ya Mombasa baada ya makasha kuanza kusafirishwa kupitia barabara ya reli ya kisasa amesema mkurugenzi wa shirika la Vijana Stretchers, Dickson Okong’o.
Mkurugenzi amedai kuwa vijana wengi waliyokuwa wakitegemea sekta ya uchukuzi wa malori wamepoteza ajira hali inayowaacha bila ya namna yoyote ya kujikimu kimaisha.
Akizungumza huko Changamwe Kaunti ya Mombasa hii leo, Okong’o ameitaja hatua hiyo kama dhuluma za kiuchumi na ambazo zinapaswa kusitishwa.
Mwanaharakati huyo wa vijana katika ameitaka Serikali kusitisha mchakato huo ili kuidhibiti sekta ya uchukuzi wa masafa marefu ambayo kwa sasa imesambaratika.
Kauli ya Okong’o inajiri huku maandamano makubwa yakitarajiwa siku ya Jumatatu kuanzia mzunguko wa barabara ya Makupa hadi Changamwe Mjini Mombasa kulalamikia ubaguzi huo wa kiuchumi.