Story by Mwanaisha/Fatuma:
Mahakama ya Kwale imeagiza mshukiwa wa ugaidi Noordin Hassan Abdallah aliyetiwa nguvuni mapema leo na maafisa wa polisi katika eneo la Majengo Kisiwani Mombasa, kuzuiliwa rumande katika gereza la Shimo la Tewa.
Hakimu mkuu wa Mahakama ya Kwale Joe Omido, ametoa agizo hilo baada ya mshukiwa huyo wa ugaidi kukosa kuhudhuria vikao vya Mahakama licha ya kuagizwa kufanywa hivyo.
Hata hivyo mdhamani wa mshukiwa huyo ambaye ni Mbunge wa Nyali Mohammed Ali amewasilisha ombi la kujiondoa katika kesi hiyo kama mdhamini wa mshukiwa huyo kupitia Wakili wake Titus Kirui, ombi ambalo Mahakama imelikubali.
Mshukiwa huyo wa ugaidi, anadaiwa kuwa mshirika wa mshukiwa mkuu wa ugaidi Salim Rashid Mohammed, ambaye ni Mwanachama wa mtandao wa kigaidi wa Islamic State IS.
Kesi hiyo hata hivyo itasikizwa Novemba 18 mwaka huu ambapo mshukiwa huyo wa ugaidi atakuwa na mda wa kuielezea Mahakama sababu zilizochangia kukosa kuhudhuria vikao vya Mahakama hapo awali.