Serikali ya kitaifa imesema usalama katika mipaka ya kenya na mataifa jirani umeimarishwa na maafisa wa kutosha kutoka vikosi mbali mbali vya usalama wametumwa maeneo hayo kupiga doria.
Katika mahojiano ya kipekee na meza yetu ya habari,msemaji wa serikali kanali mstaafu Cyrus Oguna amesema hatua hio inalenga kuzuia wahalifu kupenya humu nchini kupitia mpakani na kutatiza usalama.
Oguna vile vile amesema kwa sasa uhusiano kati ya Kenya na taifa la Somalia uko dhabiti kwani mzozo ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo umetatuliwa na sasa mataifa hayo yanalenga kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi.
Akigusia suala la kuondolewa kwa marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku linalopigiwa upato na wakenya,Oguna amesema serikali itaondoa masharti ya kupambana na corona kwa awamu ili kuzuia athari zaidi za kiafya kwa wakenya.
Oguna aidha ameeleza kuwa serikali kuu kupitia halmashauri ya barabara kuu nchini KENHA inaendeleza mipangilio ya kuhakikisha mradi wa ujenzi wa barabara ya Kwale – Kinango unakamilika kabla mwaka ujao wa kifedha.