Taarifa na Salim Mwakazi
Kwale, Kenya, Juni 24 – Wizara ya mazingira nchini imeanzisha mradi wa upanzi wa miti ya mikoko katika eneo la Pwani kama njia mojawapo ya kuhifadhi mazingira ya bahari.
Waziri wa Mazingira nchini Keriako Tobiko amesema mradi huo unalenga kuhakikisha idadi ya miti ya mikoko inayopandwa pwani inaongezeka ili kuinua uchumi wa taifa kupitia bahari.
Tobiko amesema mradi huo ambao umeanzishwa katika baadhi ya kaunti za pwani utasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Waziri huyo alikuwa akizungumza katika zoezi la upanzi wa mikoko zaidi ya elfu mbili katika eneo la Vanga huko Lungalunga kaunti ya Kwale.
Akizungumza na wanahabari baada yakukamilika zoezi la upanzi wa mikoko katika eneo hilo, waziri wa ardhi na mazingira katika kaunti hiyo Saumu Beja Mahaja amewataka wakazi kuzuia ukataji wa miti ili kutunza mazingira.
Kwa upande wake afisa wa shirika la huduma ya misitu nchini Julius Kamau amesema miti ya mikoko ina umuhimu katika uhifadhi wa mazingira akisema shirika hilo litafanya jitihada kuhakikisha mikoko inalindwa.