Story by our Correspondents –
Kenya imepokea chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona dozi 459,300 ya AstraZenaca kutoka taifa la Canada kama njia moja wapo ya kupiga jeki juhudi za kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.
Akizungumza na Wanahabarai baada ya kupokea shehena ya dozi hiyo katika uwanja wa ndege ya kimataifa wa Jomo Kenyatta, Katibu katika Wizara ya Afya nchini Susan Mochache amesema kufikia sasa Kenya imepokea dozi 4,069,900.
Mochache amesema Kenya inatarajia kupokea dozi nyingine ya chanjo ya Johnson na Johnson siku ya Ijumaa juma hili na chanjo zaidi ya milioni 4.16 katika wiki chache zijazo.
Wakati uo huo ameweka wazi kwamba chanjo hiyo inatolewa bila malipo katika vituo vyote vya afya vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya nchini huku akionya kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaolenga kuhitilafiana na zoezi la utoaji chanjo.