Mahakama kuu ya Mombasa imemuachilia huru mjane wa Marehemu Sheikh Aboud Rogo, Bi Hannia Sagar Said Rogo, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kuhusishwa na visa vya ugaidi.
Hannia Sagar Said Rogo alikuwa amehukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kushindwa kuzuia uvamizi katika kituo cha polisi cha Central mjini Mombasa mnamo tarehe 11mwezi Septemba mwaka 2016.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Dora Chepkwony amesema kifungo alichohukumiwa Mjane wa Marehemu Aboud Rogo kinakiuka Katiba na haki za mshtakiwa, ikizingatiwa kuwa washtakiwa wengine watatu waliokuwa wameshtakiwa na mjane wa Marehemu Aboud Rogo waliachiliwa huru.
Jaji Chepkwony kwenye uamuzi wake, amedokeza kuwa madai kuwa Mjane wa Rogo alipokea shilingi elfu 10 ambazo zinadaiwa kufadhili visa vya ugadi kutoka kwa mshukiwa wa ugaidi aliyeuwa katika kituo cha polisi cha Central hayana uzito wowote. Ameongeza kuwa upande wa mashtaka ulikosa kuweka wazi iwapo pesa hizo zilitumika ama zingetumika katika kununua vifaa vya kutekeleza ugaidi.
Taarifa na Hussein Mdune.