Taarifa na Mimu Mohammed
Rais Uhuru Kenyatta ametia saini miswada miwili kuwa sheria kwa lengo la kuimarisha kujitosheleza kwa chakula na matumizi bora ya ardhi nchini.
Rais ambaye hapo awali alikuwa ametia saini mswada wa unyunyizaji maji mashamba kuwa sheria, leo katika ikulu ya Nairobi, ametia saini Mswaada wa Marekebisho ya Thamani ya Ardhi,Miswada ambayo ni ya mwaka huu wa 2019.
Sheria ya unyunyizaji maji mashamba inalenga kurahisisha ustawi, usimamizi na udhibiti wa shughuli za unyunyizi, huku sheria ya thamani ya ardhi ikilenga kuleta usawa wa kubashiri thamani ya vipande vya ardhi, kodi ya nyumba, ushuru unaotozwa kugharamia shughuli za ubadilishanaji mali na kulipa ridhaa.
Sheria hiyo mpya pia inazipa mamlaka kaunti kuanzisha vitengo vya kunyunyizia maji mashamba ili kutimiza mahitaji ya kaunti binafsi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto ameandamana na Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka, Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Aden Duale na Kiongozi wa waliowengi katika bunge la Seneti Kipchumba Murkomen kuwasilisha miswada hiyo kwa Rais kuitia saini.