Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.
Jumla ya shilingi milioni 400 zinazomilikiwa na wakaazi wa Ukanda wa Pwani bado hazijachukuliwa na wenyewe licha ya fedha hizo kusalia katika Mamlaka maalum inayolinda fedha hizo ya ‘Unclaimed Financial Assets Authority’.
Afisa mkuu mtendaji wa Mamlaka hiyo John Mwangi amesema fedha hizo ni kati ya shilingi bilioni 13.1 ambazo Mamlaka hiyo inazilinda baada ya wamiliki wake kuaga dunia au kukosa kufikiwa na Mamlaka hiyo ili kukabidhiwa fedha zao.
Akizungumza Mjini Mombasa, Mwangi amesema fedha hizo huenda zilitumwa kwenye simu zao za rununu japo hakuna aliyeweza kujua nambari ya siri au watu hao waliaga dunia ghafla huku jamaa zao wakikosa habari muhimu kuhusu akaunti zao za benki, uwekezaji katika soko la hisa au kampuni za bima.
Kulingana na Mwangi, Mamlaka hiyo inaendeleza hamasa kwa wakaazi hapa Pwani kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo na kuwataka wakaazi kuwatembelea katika maonyesho ya kilimo ya Mkomani ili kufahamu mengi kuhusu malipo hayo anayosisitiza yanafanywa kwa njia ya uwazi na kwa haraka.