Picha kwa Hisani –
Mgomo wa wauguzi kaunti ya Tana-river uliodumu kwa zaidi ya siku 15 hatimaye umesitishwa.
Katibu mkuu wa muungano wa wauguzi kaunti ya Tanariver Damon Kwaraa amesema hatua hio imeafikiwa kufuatia mazungumzo yaliofanywa kati ya wahudumu wa afya na serikali ya kaunti hio.
Kwaraa amesema wamesitisha mgomo huo kwa siku 90 pekee ili kutoa nafasi kwa matakwa yao kutekelezwa kama walivyokubaliana na kwamba wamekubali kurejea kazini ili kuwaondolea mahangaiko wakaazi wa kaunti hio.
Kwaraa aidha amesema iwapo serikali ya Tana-river itashindwa kutekeleza matakwa yao katika kipindi hicho cha siku 90 watalazimika kusitisha tena shughuli zao.
Kwa upande wake, waziri wa afya kaunti ya Tanariver Javan Bonaya ameshukuru wahudumu hao wa afya kwa kukubali kurejea kazini na kwamba serikali ya kaunti hio itafanya juhudi kutimiza matakwa ya wahudumu hao.
Maafikiano hayo yametiwa saini mbele ya waziri wa fedha wa kaunti hio Mathew Babwoya na mwenyekiti wa bodi ya uajiri kaunti ya Tanariver Rashid Omar.