Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mgogoro wa umiliki wa ardhi ya shule ya msingi ya Nyali katika kaunti ya Mombasa umezuka upya huku usimamizi wa shule hiyo ukishikilia kwamba ardhi hiyo imenyakuliwa na watu binafsi.
Wakili wa shule hiyo Moses Waweru aliwasilisha stakabadhi za umiliki wa ardhi hiyo kwa kitengo cha kutatua mizozo chini ya tume ya kitaifa ya ardhi na kusema kwamba ardhi hiyo ni mali ya shule hiyo na kulikuwa na mipango ya kujengwa shule ya upili katika kipande hicho cha ardhi.
Wakili Waweru amemtaja Jaji wa Mahakama kuu Said Chitembwe kama mmoja wa watu walionyakua ardhi hiyo, huku Chitembwe kupitia kwa wakili wake Augustus Wafula ikiweka wazi kwamba alinunua ardhi hiyo kupitia kwa njia halali na mteja wake hajawahi nyakua ardhi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Mwenyekiti wa kitengo cha kutatua mizozo chini ya tume ya kitaifa ya ardhi Getrude Nguku amesema vikao vya kujadili mzozo huo wa umiliki wa ardhi hiyo vitaendelea siku ya Alhamis kabla ya Tume hiyo kutoa mwelekeo wake siku ya Ijumaa juma hili kuhusu mmiliki halali wa ardhi hiyo.
Tume ya kitaifa ya ardhi imekuwa ikiendeleza vikao vya kutanzua mizozo ya ardhi katika kaunti za Kwale na Mombasa huku ikitumia mbinu mbadala ya kutanzua migogoro badala ya kwenda mahakamani.