Huku mfumo mpya wa kidijitali wa kuwasajili wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza ukiendelezwa nchini, shule za mashinani zimeripotiwa kukabiliwa na changamoto za mtandao kufanikisha mfumo huo.
Katika shule ya upili ya Golini, kaunti ya Kwale, Naibu mwalimu mkuu wa shule hiyo Changawa Shungu Madaraka, amesema kuwa jumla ya wanafunzi 15 waliojiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo, wamesajiliwa kupitia mfumo wa zamani, na majina yao yatatumwa kwa wizara ya elimu kupitia mfumo huo mpya baadae.
Hata hivyo ameupongeza mfumo huo mpya, akisema kuwa utaziwezesha shule za viwango vya chini kupata idadi kamili ya wanafunzi waliotengewa nafasi katika shule hizo na kuchangia ushundani wa kimasomo.
Haya yanajiri huku wizara ya elimu ikiagiza usajili wa wanafunzi kupitia mfumo huo mpya kukamilika tarehe 11 mwezi huu wa Januari.
Taarifa na Michael Otieno.