Michuano ya soka ya ‘Pamba roho’ inayojumuisha timu 16 katika eneo bunge la Mvita Kaunti ya Mombasa itang’oa nanga tarehe 24 mwezi huu wa Novemba.
Kulingana na Muasisi wa Shirika la Vijana la ‘MV-CODE’ Mjini Mombasa Taib Abdulrahman kipute hicho kinazishirikisha timu kutoka maeneo ya Mji wa Kale, Bondeni, Mlango wa papa, Floringi na Mwembe tayari, huku kipute sawa na hicho kikitarajiwa kuandaliwa katika maeneo ya Majengo, Shimanzi na Tudor hivi karibuni.
Akizungumza baada ya mkao wa maandalizi ya kuanza kwa kipute hicho katika eneo la Mji wa kale, Taib amesema kwamba maleongo makuu ya kipute cha ‘Pamba roho’ ni kukuza vipaji vya Vijana wadogo na kuwawezesha kutumia vipaji vyao katika kujikimu kimaisha.
Mwanaharakati huyo wa Vijana katika eneo bunge la Mvita hata hivyo anakitaja kinyang’anyiro hicho kama kinacholiangazia swala la mihadarati na kuwakinga vijana dhidi ya uraibu wa dawa za kulevya.
Kipute hicho kinachong’oa nanga siku ya Jumamosi ya tarehe 24 mwezi Novemba mwaka huu kitakamilika tarehe 30 ya mwezi Disemba mwaka huu.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.