Picha Kwa Hisani
Siku moja tu baada ya Mbunge wa Nyali Mohammed Ali kuwasilisha hoja katika bunge la kitaifa la kutaka kutimuliwa mamlakani kwa Waziri wa Uchukuzi nchini James Macharia, sasa baadhi ya wabunge wamejitokeza na kumtetea Waziri Macharia.
Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, wamesema shtuma anazoshinikiziwa Waziri Macharia ni uongo mtupu kwani waziri huyo amewajibika vyema utendakazi wake.
Kwa upande wake Mbunge wa Buuru, Mugambi Rindikiri, amesema shtuma za kumtimua Waziri Machiria inashinikizwa na baadhi ya wafanyibiashara wa sekta ya uchukuzi wanaowatumia wanasiasa wapwani kumhujumu Macharia.
Akikosoa kauli za viongozi hao kutoka maeneo ya Mlima Kenya, Kazkazini Mashariki na Magharibi, Mbunge wa Nyali Mohammed Ali amesema hoja hiyo lazima itajadiliwa bungeni licha ya wabunge wa Pwani pia kujitega na hoja hiyo.
Naye Mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko, amekosoa kauli ya Ali kuwa kudai kuwa ameachwa pekee yake kupigania maslahi ya wapwani, akitaka swala hilo kutoingizwa siasa na badala yake hoja aliyoiwasilisha bungeni kuiweka wazi iwapo anataka kuungwa mkono na wabunge wapwani.
Katika hoja hiyo iliowasilishwa bungeni na kupokelewa na Karani wa bunge hilo Michael Sialai, inashinikiza kutimuliwa uongozi Waziri Macharia kwa kuhujumu shuhuli za uchukuzi kanda ya Pwani ikiwemo bandari ya Mombasa pamoja na sakata ya ufisadi ya shilingi bilioni 5.2 wakati akiwa Wizara ya Afya.