Mbunge wa Nyali Mohammed Ali sasa anadai kwamba Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho anamkandamiza na kumzuia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika eneo bunge lake.
Kulingana na Ali, viongozi wa kisiasa katika kaunti hiyo wamekuwa wakihitilafiana na mchakato wa maendeleo katika eneo bunge la Nyali, hali anayosisitiza kwamba hataikubali.
Akizungumza katika eneo bunge lake, Ali amemtaka Gavana Joho pamoja na Maafisa wengine wa Serikali yake kutohitilafiana na miradi ya maendeleo hususan ile inayofungamana na sekta ya elimu katika kaunti hiyo.
Kauli yake imejiri baada ya Maafisa wa polisi kuutibua mkutano wake asubuhi ya leo alipokuwa akiwakabidhi baadhi ya walimu wakuu wa shule za upili katika eneo bunge la Nyali hundi ya thamani ya shilingi milioni 35 fedha za basari.