Picha kwa hisani –
Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 4 au pesa taslimu shilingi milioni 2, huku mlinzi wake Geoffrey Otieno akiachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 1 au pesa taslimu shilingi milioni 1.5.
Wawili hao wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya Ngumbao Jola katika uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda kule Malindi Oktoba 15 mwaka wa 2019.
Jaji wa Mahakama kuu Njoki Mwangi ameamuru wawili hao kusalimisha vyeti vyao vya usafiri Mahakamani na kuwataka kutoa sababu muhimu za kusafiri nje ya nchi kabla ya wao kuruhusiwa kusafiri.
Jaji Mwangi amewatahadharisha wawili hao dhidi ya kuwatishia maisha mashahidi baada ya upande wa mashtaka unaoongozwa na Naibu Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya Umma Alloys Kemo kushikilia kuwa Jumwa ana ushawishi mkubwa na huenda akawatishia maisha mashahidi.
Hata hivyo, Mawakili wa Jumwa na Otieno wakiongozwa na Cliff Ombeta wamesema kauli ya Kemo ni njama ya kumhangaisha Jumwa akifahamu wazi kuwa mteja wake hakuhusika katika mauaji ya Jolla.