Mbunge wa Magarini kaunti ya Kilifi Michael Thoya Kingi ameahidi ujenzi wa maktaba na maabara katika shule zote za upili ambazo zinakumbwa na changamoto hiyo katika eneo hilo.
Ni baada ya kubainika kwamba shule nyingi huko Magarini hazina maabara na maktaba hali inayodaiwa kuchangia pakubwa matokeo duni ya mitihani ya kitaifa.
Kingi amewataka walimu kujitokeza kwa wingi kutoa maoni wakati kamati ya hazina ya ustawishaji wa eneo bunge (CDF) eneo hilo, itakuwa ikizunguka kukusanya maoni kuhusu miradi ya maendeleo ili kubaini miradi inayofaa kupewa kipaumbele.
Wakati uo huo, mbunge huyo wa Magarini amedokeza kuwa jumla ya shilingi milioni 11 zimetengwa kupitia ufadhili wa hazina ya CDF kwa ujenzi wa bweni kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ualimu katika chuo cha mafunzo ya ualimu cha Galana huko Magarini.
Taarifa na Esther Samini.