Story by: Mwahoka Mtsumi
Bunge la kitaifa limejadili hoja ya kupiga marufuku ndoa za mapenzi ya jinsia moja humu nchini iliyowasilishwa kwa mara ya tatu na Mbunge wa Nyali Mohamed Ali katika bunge hilo.
Akiwasilisha hoja hiyo bungeni, Mbunge wa Nyali Mohamed Ali amesema ni kinyume na mafunzo ya mwenyezi Mungu katika taifa lolote ile kuruhusu mapenzi ya jinsia moja, huku akisema kama viongozi hawatakubali uovu huo kwani tayari taifa jirani la Tanzania na Uganda zimepiga marufuku tabia hiyo.
Naye mbunge wa Laikipia Kazkazini Sarah Korere amesema kuna haja ya serikali kuwatazama kwa kina majaji wa Mahakama ya upeo walioruhusu watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja nchini kuunda chama cha kutetea maslahi yao.
Kwa upande wake mbunge wa Matuga Kassim Sawa Tandaza ameunga mkono hoja hiyo, akisema tabia hiyo ni ya kishetani huku akisisitiza kwamba ni jukumu la serikali kujitokeza na kupiga marufuku swala hilo ili kulinda kizazi kichanga.
Wakati uo huo mbunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya ambaye pia ni Naibu kiongozi wa wengi bungeni, ameonekana kukinzani na kauli za wabunge hao kuhusu hoja hiyo na jinsia katiba inayoangazia, akiwataka wabunge kuielewa vyema katiba kuhusu uhuru wa kujieleza
Hata hivyo Spika wa zamu Martha Wangari ambaye pia ni Mbunge wa Gilgil amefafanua zaidi hoja hiyo kwa kuambatana na Katiba ya nchi ambayo inakataza ndoa za jinsia moja humu nchini.