Swala la nidhamu miongoni mwa vijana katika Kaunti ya Mombasa linapaswa kutiliwa mkazo sio tu katika mazingira ya shuleni bali pia nyumbani.
Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir ameitaja hali hiyo kama tata mno akihoji kwamba vijana wengi wamepotoka kinidhamu na kimaadili hali inayowasukuma katika maovu.
Akizungumza katika eneo bunge lake la Mvita, Nassir amesema iwapo vijana hawatafunzwa nidhamu na kuelekezwa katika maadili mema maswala ya uraibu wa dawa za kulevya na uhalifu miongoni mwao kamwe hayatadhibitiwa.
Kulingana na kiongozi huyo, ni sharti jamii na viongozi waungane katika kuandaa makongamano ya vijana na kuwaelekeza vijana katika njia njema kwa lengo la kuwakinga na maovu katika jamii.
Nassir ambaye amekabidhiwa uongozi wa Chama cha Maskauti katika kaunti ya Mombasa ameapa kuandaa makongamano ya vijana mashinani ili kuhimiza nidhamu na maadili mema miongoni mwao.