Story by Mimuh Mohamed –
Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i amefika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa kuhusu usalama kuhojiwa kuhusiana na usalama wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto baada ya walinzi katika makaazi ya Ruto kubadilishwa.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Matiang’i amesema wizara ya usalama wa ndani ilizingatia sheria na utaratibu ufaao katika kuwaondoa maafisa wa GSU katika makaazi ya Ruto na kuwaweka maafisa tawala kulinda maeneo hayo.
Matiang’i kwenye maelezo yake, amesema Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake wanalindwa na maafisa wa kitengo maalum na waliopewa mafunzo ya kutosha akihakikishia wakenya kwamba usalama wa Ruto uko imara.
Wakati huo huo amesema hana ufahamu wa matukio yaliotekelezwa hivi karibuni na wizara hiyo yanayohatarisha maisha ya Naibu wa Rais akisema kiongozi huyo analindwa na maafisa wa 257, ambapo maafisa 74 ni wale wa kuongoza msafara wa rais, maafisa 5 wa GSU kutoka kitengo maalum, 6 wa idara ya ujasusi, 121 wa utawala kutoka kitengo maalum ikiwemo maafisa wengine.