Story by Our Correspondents-
Waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i amesema usalama wa taifa umeimarishwa ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi huu unaandaliwa kwa amani.
Katika kikao na wadau wa kiusalama, Waziri Matiang’i amewataka wakenya kutokuwa na hofu yoyote kwani maafisa wa usalama watatumwa mashinani kulinda maisha ya wananchi hasa wakati huu wa uchaguzi mkuu.
Matiang’i amesema taifa limeshuhudia utulivu na amani kwa miaka mingi na itakuwa vyema iwapo wakenya wataendelea kuishi kwa uwiano na utangamano huku akiwaonya wanasiasa dhidi ya kuchochea siasa za vurugu.
Akigusia sintofahamu za kisiasa katika eneo la Bonde la Ufa, Waziri Matiang’i, amesema idara ya usalama imejipanga vyema kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanashiriki uchaguzi wa amani huku akiwataka kutokuwa na hofu yoyote ya kiusalama.
Wakati uo huo amewataka maafisa tawala ikiwemo machifu, manaibu wao, makamishna wa kaunti na maafisa wengine kujitenga na kauli za wanasiasa wasio na malengo bora kwa wakenya na kuwajibikia majukumu yao ya kiserikali ya kuimarisha usalama.