Story by Our Correspondents-
Waziri wa usalama nchini Dkt Fred Matiang’i amesema serikai itahakikisha inaimarisha usalama wa wananchi kote nchini ili kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa njia ya amani.
Akizungumza katika kikao cha usalama katika kaunti ya Marsabit ambapo hivi majuzi kulishuhudia uvamizi kutoka kwa baadhi ya makundi ya kihalifu katika kaunti hiyo, Matiang’i ameshikilia kwamba serikali itatuma maafisa wa kutosha nyanjani.
Matiang’i ameshikilia kwamba serikali haitaruhusu wananchi wakiendelea kuhangaishwa na wahalifu kila mara, akisema ni lazima kaunti hiyo ishuhudie amani na usalama kwani baadhi ya maeneo katika kaunti hiyo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama.
Kauli yake imeungwa mkono na Inspekta jenerali wa polisi nchini Hillary Mutyambai, aliyesema ni lazima usalama wa nchi ulindwe huku akiwahimiza wananchi kuwaripoti wahalifu kwa polisi.