Wizara ya elimu nchini imetakiwa kuingilia kati kuboresha miundo msingi ya shule ya msingi ya Mangororo katika eneo bunge la Ganze kaunti ya Kilifi.
Mwito huu umetolewa baada ya masomo kukatizwa katika shule hiyo kutokana na kujaa maji kwa madarasa.
Akiongea na wanahabari katika Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 300 mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Patos Baya amesema kuwa shule hio inahitaji msaada wa dharura wa ujenzi wa madarasa madhubuti kwani baadhi ya wanafunzi wanasomea chini ya miti.
“Jengo lenyewe haliwezi kustahimili, mvua ikinyesha maji yanaingia ndani. Ukiangalia huku upande mwingine watoto wanakaa kwenye mawe. Kwa hivyo shule unauhitaji mkubwa wa madarasa. Hususan madarasa kama sita,” amesema Baya.
Mwenyekiti wa chama cha waalimu na wazazi PTA katika shule hiyo Justus Mwaringa amesema shule hiyo haina madawati hali inayochangia wanafunzi wa shule hio kupata matokeo duni.
Mwaringa amewanyoshea kidole cha lawama viongozi wa eneo hilo kwa kutoboresha miundo msingi ya shule hio.
“Kusema kweli hii shule haina dawati hata moja, viongozi wetu nakosa kuwaelewa,kuna kwengine shule zinaendelea vizuri lakini viongozi wetu nakosa kuwaelewa. Kwani hii shule haiku Kenya?” ameuliza Mwaringa.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Getrude Nyambu amekiri kwamba shule hiyo ina mazingira duni akiwataka wadau husika kuingilia kati kutatua tatizo hilo.
Taarifa na Charo Banda.