Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mashirika yasiokuwa ya kiserikali Kanda ya Pwani yamepinga uamuzi wa mahakama kuu uliyotupilia mbali kesi yao ya kutaka sheria ya kukabiliana na ugaidi nchini ifanyiwe marekebisho.
Watetezi hao wakiongozwa na Afisa mkuu wa maswala ya dharura katika Shirika la MUHURI Francis Auma wamesema jinsi sheria hiyo ilivyo itasambaratisha utendakazi wa mashirika hayo na kuipatia Serikali mamlaka ya kudhulumu wananchi.
Auma amesema ni sharti sheria hiyo ifanyiwe marekeibisho ili isiwe kandamizi kwa upande wowote ule.
Auma amesema kwamba wakereketwa hao wa maswala ya haki za kibinadamu watakata rufaa mahakamani ili kuzuia utekelezaji wa sheria hiyo hadi ifanyiwe marekebisho.
Katika sheria hiyo, kituo cha kupambana na ugaidi nchini NCTC kimepewa majukumu ya kusimamia shughuli zote za mashirika yasiyokuwa ya kiserikali humu nchini na kimataifa hali ambayo itatatiza hata ufadhili wa mashirika hayo.
Hata hivyo, Jaji wa mahakama kuu Mjini Mombasa Eric Ogola ametupilia mbali kesi iliyowasilishwa na mashirika hayo ya kutaka sharia hiyo ifanyiwe marekebisho akisema kamwe haitawaathiri wakereketwa hao.