Mashirika yanayoangazia maswala ya amani, na usalama hapa Pwani yameitaka Idara ya usalama kaunti ya Kilifi kuidhinisha mjadala wa kiusalama kuhusu swala la kuuwawa kwa wazee kwa tuhuma za uchawi.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kijamii la KECOSCE, Phyllis Muema amesema swala hilo tata halionekani kukomeshwa hivi karibuni, huku akitaka jitihada zaidi kuwekezwa ili kukomesha ukiukaji huo wa haki za kibinadamu.
Akizungumza wakati wa maandalizi ya maadhimisho hayo mjini Kilifi, Phyllis amesema hali tata ya kampuni za uchimbaji mawe na utengenezaji saruji zinavyowahangaisha wakaazi katika kaunti ya Kilifi inastahili kuangaziwa.
Mwanaharakati huyo hata hivyo amedokeza kuwa japo kubadilishwa kwa sare za Maafisa wa polisi ni jambo la busara, hali hiyo haitoshi katika kuwashinikiza Maafisa wa usalama kuwajibikia majukumu yao.
Maadhimisho hayo ya siku ya amani ulimwenguni yatafanyika mjini Kilifi hapo Kesho.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.