Story by Ali Chete –
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yameibuka na mikakati itakayohakikisha wanaohusika katika kueneza uchochezi wakati wa uchaguzi wanatiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka.
Mashirika hayo yakiongozwa na Mwenyekiti wao Simon Kazungu yamesema kufuatia kauli za baadhi ya wanasiasa huenda zikachangia vurugu za kisiasa humu nchini na kuitaka idara ya usalama kuhakikisha inawajibikia majukumu yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu Muungano wa vuguvugu la First Action Movement Harriet Muganda amewataka wanasiasa kukoma kuwatumia vijana vibaya kwa manufaa yao binafsi.
Kauli zao zimeungwa mkono na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Haki Africa Hussein Khalid aliyesema kama mashirika wameweka mikakakti ya kuhakikisha taifa linashuhudia amani ikiwemo kununua kamera fiche za kunasa sauti na video kwa viongozi wachochezi.