Story by Janet Shume-
Mashirika mbalimbali ya kijamii yamependekeza ngazi zote za serikali kushirikiana ili kuweka mpango wa kusambaza sodo katika shule za msingi na sekondari katika kaunti ya Kwale.
Mashirika hayo yakiongozwa na Shirika la Adis Clinic kupitia afisa wake wa Afya Caroline Wanjiru amesema hatua hiyo itapunguza visa vya wasichana kukosa masomo nyakati za hedhi.
Caroline amesema wasichana wengi kutoka jamii zisizojiweza hususan eneo bunge la Kinango na Lungalunga katika kaunti hiyo wameacha shule kutokana na ukosefu wa sodo.
Wakati uo huo ameitaja hali hiyo ya wasichana kusalia nyumbani kutokana na ukosefu wa Sodo kupelekea baadhi yao kuingia katika ndoa za mapema pamoja na kuajiriwa ili kuwasaidia wazazi na majukumu ya kinyumbani hali ambayo ni kinyume cha sheria.