Huku Maandalizi ya maonyesho ya kitaifa ya Kilimo ya mwaka huu yakikaribia kukamilika, idadi ya mashirika yaliyojisali kushiriki katika maonyesho hayo kufikia sasa imeongezeka hadi 190 kutoka150 mwaka uliopita.
Kwenye mkao na wanahabari katika uwanja wa maonyesho hayo kule Mkomani kaunti ya Mombasa, Mwenyekiti wa maonyesho hayo Anisa Abdallah amesema idadi hiyo huenda ikaongezeka kwani bado mashirika zaidi yanaendelea kujisajili.
Anisa ametoa wito kwa wakaazi wa Mombasa hasa vijana kujitokeza kwa wingi katika maonyesho hayo, akisema yanapania kutoa mafunzo ya kuboresha Kilimo, kupanua biashara na kuongeza ujuzi katika ubunifu wa Kilimo biashara.
Wakati uo huo amedokeza kuwa wanatarajia wawekezaji zaidi kujisajili katika maonyesho hayo huku akisema mataifa ya nje kama vile Uganda, Uchina na Ukraine yataweza kuonyesha bidhaa zao mpya za Kilimo kwa wakulima mbalimbali. Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufungua ramsi maonyesho hayo ya kimataifa ya Kilimo tarehe 30 mwezi huu.
Taarifa na Hussein Mdune.