Picha kwa hisani –
Maseneta wa chama cha Jubilee wanakutana katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi na rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuhutubia kwenye kikao hicho.
Akizungumzia kikao hicho seneta wa kericho Aron Kipkirui Cheruiyot amesema bado hawajafahamishwa ajenda ya mkutano huo na kwamba katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amewataka kusubiri kupewa nakala za ajenda za kikao hicho.
Cheruiyot hata hivyo amesema wamepata fununu kwamba kwenye kikao hicho Jubilee inapanga kumvua mamlaka kiranja wa wengi katika bunge la seneti Irungu Kang’ata baada ya kutofautiana na rais Uhuru Kenyatta kuhusu mswada ya BBI.
Kwa upande wake seneta wa Meru Mithika Linturi amesema kwenye ujumbe mfupi wa mualiko waliotumiwa haukutoa maelezo kuhusu ajenda za mkutano huo na kwamba iwapo wanapanga kumbandua Kanga’ata lazima sheria izingatiwe.
Naye Irungu Kang’ata aliyekiranja wa wengi katika bunge la seneti amesema hajafahamishwa kuhusu ajenda ya kutimuliwa kwake na kwamba yuko tayari kwa uamuzi utakaotolewa na chama cha jubilee dhidi yake.