Picha kwa hisani –
Mashahidi wa gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko wamefika mbele ya seneti kutoa ushahidi wao dhidi ya madai yanayomkabili gavana huyo madai yaliopelekea kubanduliwa kwake mamlakani na wawakilishi wadi wa bunge la Nairobi.
Akitoa ushahidi wake Sylvia Museiya ambae ni mwakilishi wa wadi kaunti ya Nairobi amesema kubanduliwa kwa gavana sonko hakukuzingatia sheria kwani baadhi ya wawakilishi wa wadi waliorodheshwa kati ya wale waliounga mkono hoja hio licha ya kutoshiriki mchakato huo.
Shahidi wapili Emmanuel Karisa Kenga ambae ni mtaalamu wa kukagua nakala,amesema baadhi ya saini zilizowekwa kwenye orodha ya wawakilishi wadi waliounga mkono hoja ya kubanduliwa kwa sonko hazikua halali.
Akijitetea mbele ya maseneta gavana Sonko amepinga madai ya kufuja shilingi milioni 297 pesa za basari za mwaka wa kifedha 2018-2019, akisema fedha hizo zilitumika kama ilivyopangwa kinyume na wanavyodai wajumbe wa Nairobi.
Baada ya sonko kujitetea dhidi ya shutuma za ubadhirifu wa fedha za umma na utumizi mbaya wa ofisi,maseneta 47 wataipigia kura hoja ya kubanduliwa kwake,na atahitaji kura 24 ili kupona shoka la kubanduliwa mamlakani.