Story by Our Correspondents –
Marjan Hussein Marjan ameapishwa rasmi kuwa Afisa mkuu mtendaji wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC baada ya kushikilia nafasi hiyo kama Kaimu kwa mda wa miaka mitatu.
Halfa hiyo ya kuapishwa kwa Marjan imetekelezwa na Jaji mkuu nchini Martha Koome katika majengo ya Mahakama ya Upeo na kushuhidiwa na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliyeandamana na makamishna wa tume hiyo.
Wakati wa halfa hiyo Marjan ameahidi kuhakikisha anazingatia katiba ya nchi sawa na sheria zengine za umma, pamoja na kuwa muaminifu katika majukumu yake ya kazi na kuwatumikia wakenya vyema.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo Jaji mkuu nchini Martha Koome, amewahimiza makamishna wa tume hiyo chini ya Mwenyekiti wao Wafula Chebekati kuhakikisha taifa linashuhudia uchuguzi huru na haki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, amewaahidi wakenya kwamba tume hiyo imejiandaa vyema kuhakikisha inafanikisha uchaguzi huru na haki huku akiweka wazi kwamba ukaguzi wa sajili ya wapiga kura unaendelea na tume hiyo iko tayari kushirikia na idara ya Mahakama.