Mahakama kuu Mjini Malindi imewawachilia huru kwa dhamana ya shilingi milioni moja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho Maafisa wawili wa polisi wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Mwanafunzi Katana Kazungu.
Hata hivyo jaji wa Mahakama kuu ya Malindi Reuben Nyakundi amesema kwamba ni lazima mahakama idhibitishe wadhamini wa Maafisa hao wawili wanaokabiliwa na mauaji kabla ya kuwawachilia huru kwa dhamana.
Maafisa hao wawili Simeon Ayodo na Amos kipsang wanakabiliwa na mauaji ya Mwanafunzi Katana Kazungu aliyekuwa na umri wa miaka 17 na Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi ya Ndatani huko Kaloleni Kaunti ya Kilifi mwezi Juni mwaka uliyopita.
Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI lilishirikiana na tume inayochunguza maswala ya polisi nchini IPOA katika kesi hiyo, juhudi zilizopelekea wawili hao kuwachishwa kazi, kutiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka.
Hata hivyo wawili hao walikanusha mashtaka hayo na kesi yao itaendelea tarehe 8 mwezi ujao wa Aprili.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.