Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mamlaka ya ushuru nchini KRA imepanda jumla ya mikoko 16,000 katika mkono wa bahari hindi wa Mchenjamaisha katika eneo la Jomvu kaunti ya Mombasa.
Afisa wa Mamlaka hiyo kanda ya Pwani Simon Mwaniki amesema juhudi hizo zinatokana na hali tata ya kimazingira inayoikumba nchi na inayostahili juhudi za washika dau katika kuizima hali hiyo.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Mwaniki amesema iwapo kila Mkenya atajitahidi na kuchukua jukumu la kulinda mazingira basi taifa hili litashuhudia hali bora zaidi ya mazingira kwa kila mmoja kuishi.
Mwaniki amesema halmashauri hiyo ikishirikiana na wadau wengine nchini imekuwa ikiendeleza shughuli za upanzi wa miti katika maeneo mbalimbali ya Pwani ili kuafikia asilimia 10 ya misitu kote nchini.
Aidha amewataka wakaazi wa Ukanda wa Pwani kukumbatia upanzi wa miti katika juhudi za kulinda mazingira kadri taifa linavyoshuhudia mabadiliko ya hali ya anga na ukame kufuatia ukosefu wa mvua.