Story by Ali Bakari-
Hakimu mkuu wa mahakama ya Mombasa Martha Mutuku, Hakimu mkuu mwandamizi wa mahakama hiyo Martin Rabera na wanaharakati kutetea haki za binadamu katika kaunti ya Mombasa walizawadiwa tuzo za utendakazi bora zilizoandaliwa na Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Huria.
Akizungumza wakati wa kuwazawadi washindi hao, Mkurugenzi wa shirika hilo Francis Kariuki amesema tuzo hizo zinalenga kuboresha utendakazi wa idara ya mahakama katika kanda ya Pwani sawa na ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu nchini
Kwa upande wake Afisa wa masuala ya kisheria katika shirika hilo Antony Maghanga amesema hatua hiyo itasaidia katika ufahamu wa kisheria kwa jamii na ushirikiano kati ya idara ya mahakama na wadau wengine.
Naye Hakimu mkuu mwandamizi wa mahakama ya Mombasa Martin Rabera na mwanaharakati wa kijamii katika kaunti hiyo John Tsuma waliyoibuka na ushindi katika tuzo hizo wamepongeza juhudi za shirika hilo katika kuleta ushirikiano huo, wakisema utaleta uhusiano mwema kati ya jamii, idara ya mahakama na wadau wengine wa masuala ya kisheria.