Story by Mimuh Mohamed-
Mahakama ya kutatua mizozo ya uajiri na leba imeizuia kwa muda Tume ya huduma za umma nchini PSC, dhidi ya kuidhinisha afisi ya katibu mkuu muandamizi maarufu CAS.
Jaji wa Mahakama hiyo Monica Mbaru ametoa uamuzi huo kufuatia kesi iliyowasilishwa na chama cha mawakili nchini LSK, akisema muelekeo kuhusu afisi ya CAS utatolewa baada ya kesi hiyo kuamuliwa.
Jaji Mbaru katika uamuzi wake vile vile ameagiza chama cha LSK kuikabidhi tume ya huduma za umma nchini pamoja na mkuu wa sheria nchini nakala kuhusu kesi hiyo kabla Oktoba 14 huku kesi hiyo ikitarajiwa kusikilizwa tarehe 24 mwezi huu.
Katika kesi hiyo LSK imelalamika kutokua na uwazi kuhusu majukumu ya afisi ya CAS kwani kunawanyima wananchi fursa ya kutoa maoni kuhusu uwezekano wa kufanana kwa majukumu kati ya afisi ya CAS na ile ya makatibu.
Uamuzi huo wa Mahakama hata hivyo unajiri huku Tume ya huduma za umma nchini kupitia Mwenyekiti wake Antony Muchiri ikiwa tayari imewataka wakenya kutuma maombi ya kujaza nafasi hizo za CAS.