Mahakama kuu mjini Malindi imetupilia mbali kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire kwenye uchaguzi mkuu uliopita, kesi iliyowasilishwa na Mlalamishi Mubaruk Issa Kombe.
Akitoa uamuzi huo Jaji wa Mahakama hiyo Erick Ogola, amesema upande wa mlalamishi ulikosa kutoa ushahidi wa kutosha ambao ungepelekea kubatilisha kuchanguliwa kwa mbunge wa sasa.
Jaji Ogola ametoa muda wa siku 14 kwa mlalamishi wa kesi hiyo Mubaruk Issa Kombe kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi wa Mahakama huku Mahakama ikimuagiza mlalamishi huyo kulipa shilingi milioni 2.5 kama gharama ya kesi hiyo.
Akiongea na Wanahabri nje ya Majengo ya Mahakama hiyo, Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire aliyekuwa ameandamana na viongozi mbali mbali wa chama cha ODM akiwemo Mbunge wa Saboti Caleb Khamis, Seneta wa Kwale Issa Boi, Seneta wa Mombasa Mohammed Faki miongoni mwa viongozi wengine amepongeza uamuzi wa mahakama hiyo, akiwataka viongozi wenza kuweka kando tofauti zao za kisiasa.
Taarifa na Esther Mwagandi.