Mkurugenzi wa shirika la kupambana na dawa za kulevya na vileo nchini Pwani (NACADA), Farida Rashid, ameitaka idara ya mahakama kuacha kutoa faini ndogo kwa walanguzi wa mihadarati. Picha/ Gabriel Mwaganjoni
Taarifa na Charo Banda.
Malindi Kenya, 22 Mei – Shirika la kupambana na dawa ya kulevya na vileo haramu nchini (NACADA), sasa linaitaka idara ya mahakama kuwajibika kikamilifu katika vita dhidi ya mihadarati humu nchini.
Mkurugenzi wa Shirika hilo kanda ya Pwani Farida Rashid, amesema mahakama imechangia pakubwa kuzorota kwa juhudi hizo kutokana na hukumu ndogo ndogo inazotoa kwa walanguzi wa dawa za kulevya wanapofikishwa mahakamani.
“Tumepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi. Wanasema watu wanashikwa wakiuza mihadarati na wakifikishwa mahakamani wanaachiliwa kwa faini ndogo sana. Mahakama ijue kufanya kazi yake vizuri ijue kuhukumu wale wanaouza mihadarati maanake wanauwa watu, watoto wetu wanaangamia,”amesema Bi Farida.
Kauli yake imeungwa mkono na mwanaharakati wa kupambana na mihadarati ukanda wa Pwani Famau Mohamed Famau ambaye amesisitiza haja ya mahakama kuwajibika kikamilifu kuhusu kesi zote za washukiwa wa madawa ya kulevya.
“Tungeomba mahakama itoe adhabu kali kwa wale ambao ni wauzaji wa madawa ya kulevya. Kuliko kuwapa vifungo vidogo au faini ndogo,” amesema Famau.
Famau ameongeza kuwa huenda baadhi ya vijana ambao tayari wamejitosa katika katika utumizi wa dawa za kulevya wakosa kuoa na kuwa na familia katika siku zijazo iwapo swala hilo halitashuhulikiwa.