Story by Gabriel Mwaganjoni –
Mahakama ya Mombasa imewapata na hatia ya kutolipa ushuru wafanyibiashara watatu baada ya kuingiza bidhaa zao humu nchini.
Mahakama imethibitisha kwamba wafanyibiashara hao akiwemo Maur Bwanamaka Abdallah, Ali Mohammed Ali na Abdullah Hussein Mer walishirikiana katika kuingiza sukari na vyuma vikuu kuu kutoka Zanzibar mnamo tarehe 28 mwezi Oktoba mwaka 2019.
Wakiwa mbele ya Hakimu mkuu wa Mahakama ya Mombasa Edna Nyaloti, amesema watatu hao wanadaiwa waliingiza sukari waliyotaja kuwa mchele wa magunia 1,000 pekee ya kilo 25 na tani walizodai kuwa 10 za vyuma vikuu kuu.
Bwanamaka ambaye ni Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya uwakala wa forodha ya Federal Commercial Investments, Ali Mohammed Ali akiwa Mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Captain Shipping Agency na Abdulla Hussein Mer akiwa nahodha wa meli ya Mv-Al Fazal walikwepa kulipa ushuru wa shilingi milioni 13.1.
Hata hivyo baada ya uchunguzi wa Mamlaka ya ushuru nchini KRA, ilibainika kuwa idadi kamili ya magunia hayo ya sukari yalikuwa 15,045 huku vyuma vikiwa jumla ya tani 16, mali yote ikiwa ya thamani ya shilingi milioni 22.5.
Hakimu Nyaloti amemtaka kiongozi mkuu wa mashtaka kutoa ripoti ya watatu hao iwapo wana kesi nyingine mahakamani, au ikiwa meli hiyo bado ingali katika bandari ya Mombasa au ikiwa mali yote ingali katika bandari hiyo kabla ya kutoa hukumu kwa watatu hao.
Hata hivyo hukumu dhidi ya kesi ya watatu hao itatolewa tarehe 7 mwezi Juni mwaka huu.