Story by Rasi Mangale-
Mahakama kuu ya Mombasa imeiagiza Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kumuidhinisha Mike Mbuvi Sonko kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa Agosti 9.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo akiwemo Jaji Anne Ong’injo, Stephen Githinji na Olga Sewe wameiagiza IEBC kujumuisha jina la Sonko katika orodha ya majina ya wagombea wa ugavana wa Mombasa na kulichapisha rasmi katika gazeti la serikali.
Jopo hilo la majaji, limeshikilia kwamba IEBC ilikiuka sheria kwa kumtupa nje ya kinyang’anyiro cha ugavana wa Mombasa Mike Mbuvi Sonko, wakisema taratibu zilizotumika zimekosa kuweka wazi sababu kuu za mwanasiasa huyo kutowania kiti hicho.
Hata hivyo Tume ya IEBC kupitia Mawakili wake wakiongozwa na Wakili Edwin Mukele wamesema watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo, wakidai kwamba kiongozi huyo haifai kuwania ugavana wa Mombasa kwa mujibu wa kipengee cha 75 cha Katiba.
Itakumbukwa kwamba Mnamo tarehe 23 mwezi Juni mwaka huu, Sonko alienda Mahakamani kusimamisha chama cha Wiper kutowasilisha majina ya wagombea wengine kwa IEBC sawa na tume hiyo kutochapisha makaratasi ya wagombea wa ugavana wa Mombasa hadi kesi yake kusikilizwa na kuamuliwa.