Story by Gabriel Mwaganjoni –
Mahakama kuu mjini Mombasa imetupilia mbali ombi la Afisa mkuu mtendaji wa bodi ya huduma za maji Pwani Jacob Kimutai Torutt aliyetaka kuongozewa muda wa kuhudumu kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.
Jaji wa Mahakama kuu Byram Ongaya amesema muda wa Torutt kuhudumu katika bodi hiyo tayari ulikamilika na uteuzi wa Afisa mkuu mtendaji mpya unafaa kufanywa.
Mnamo mwezi Mei mwaka wa 2020, Torutt aliongozewa muda wa mwaka mmoja kuhudumu katika bodi hiyo baada ya muda wake wa miaka mitatu kukamilika.
Hata hivyo, Afisa huyo aliwasilisha kesi Mahakamani mnamo Aprili tarehe 12 mwaka huu, akitaka kuongezewa muhula mpya wa miaka mitatu ili aendelee kuhudumu.
Hata hivyo, Jaji Ongaya amezima ndoto hiyo akitaka uteuzi mpya ufanywe huku Omar Boga akisalia kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo.