Story by Jeff Ngombo-
Mwanamume wa umri wa miaka 28 amefikishwa katika Mahakama ya Malindi, kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wawili wa kiume katika eneo la Kisumu ndogo mjini Malindi.
Mahakama imeelezwa kwamba mshukiwa kwa jina Patrick Mbauni Muriithi aliwanajisi watoto hao kati ya tarehe moja Disemba mwaka 2021 na tarehe moja mwezi Agosti mwaka 2022, wakati akihudumu kama mkufunzi wa timu ya mpira ya watoto hao.
Akiwa mbele ya Hakimu mkuu wa Mahakama hiyo Elizabeth Usui, mshukiwa amekana shtaka hilo pamoja na mashtaka mengine tisa ya dhulma za kijinsia kwa watoto hao yanayomkabili.
Upande wa mashtaka umeiomba Mahakama kuwapa muda wa siku 14 kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mashtaka hayo kabla ya kutoa ripoti kuhusu iwapo mshukiwa anapaswa kuachiliwa kwa dhamana au la.
Hata hivyo Hakimu Elizabeth amelikubali ombi la upande wa mashtaka na kuamrisha jamaa huyo kuzuiliwa hadi tarehe 7 mwezi Februari wakati ripoti ya uchunguzi wa mashtaka hayo itakapowasilishwa Mahakamani.