Story by Gabriel Mwaganjoni –
Mahakama kuu mjini Mombasa imeamuru jumla ya makasha 82 yanayodaiwa kuwa na majani chai meusi kukaguliwa upya kabla ya kukabidhiwa mmiliki wake, baada ya mamlaka ya ushuru nchini KRA kutilia shaka majani chai hayo.
Jaji wa Mahakama hiyo John Mativo amesema mmiliki wa makasha hayo ambayo ni kampuni ya Cup of Joe Limited iliiambia mahakama kwamba majani chao hayo yalifaa kupakuliwa na kisha kuchanganywa kitaalam na majani chai ya humu nchini kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje.
Tayari makasha mawili yamekaguliwa kabla ya mmiliki wa mali hiyo kufika mahakamani akipinga zoezi hilo, japo mahakama ikaamuru zoezi kuendelea kwa kipindi cha siku 14 sawa na ukaguzi huo kufanywa kwa makasha 4 kila siku.
Hatua hiyo inafuatia kauli ya mkuu wa sheria nchini la kudai kwamba huenda biashara hiyo inahusishwa na ufadhili wa shughuli za kigaidi kwani idara ya ujasusi nchini ilikuwa imetoa taarifa kuhusu shughuli za kampuni hiyo ya Cup of Joe Limited.
Bidhaa hizo ziliingizwa humu nchini kutoka nchini Vietnam na Iran kati ya mwezi Aprili tarehe 13 mwaka wa 2021 na tarehe 13 mwezi Juni mwaka uo huo licha ya kampuni hiyo ya Cup of Joe Limited kusema kwamba ilihusisha Shirika la majani chai la KTDA, huku Shirika hilo limesema halina ufahamu wowote kuhusu bidhaa.