Mombasa Kenya, Mei 28 – Mahakama ya rufaa mnamo tarehe 26 mwezi Septemba mwaka huu itaamua iwapo kesi kuhusu usimamizi wa bandari ya Mombasa itaendelea kusikizwa au.
Majaji watatu wa mahakama hiyo Patrick Kiage, Mohammed Warsame na Agnes Murgor wameiambia mahakama hiyo kwamba watatoa uamuzi wao Septemba tarehe 26 baada ya Wakaazi watatu wa Kaunti ya Mombasa William Ramogi, Gerald Kitti na Asha Omar walitaka ufafanuzi wa kikatiba kuhusu umiliki wa Bandari ya Mombasa.
Watatu hao wanataka usimamizi wa Bandari ya Mombasa usimamiwe na Serikali ya Kaunti ya Mombasa wakisema kwamba kuhamishwa kwa shughuli nyingi za ukaguzi na kupasishwa makasha katika Bandari ya Mombasa umehamishiwa katika bandari kavu ya ‘Inland Container Terminal’ Jijini Nairobi.
Watatu hao wanasema kwamba kupelekwa kwa shughuli nyingi za Bandari ya Mombasa katika eneo hilo la kuegesha makasha Jijini Nairobi kumepelekea shughuli nyingi katika sekta ya uchukuzi wa makasha kupitia barabara ya lami kufungwa baada ya maafikiano kati ya Bandari ya Mombasa na Shirika la reli nchini kwamba makasha yasafirishwe kupitia barabara ya reli ya kisasa SGR.