Story by our Correspondents –
Mahakama kuu imedinda kutoa agizo la kuzuia kuapishwa kwa makamishna wanne wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC walioteuliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta.
Katika uamuzi wake Jaji wa Mahakama kuu Weldon Korir amesema ushahidi uliyowasilishwa Mahakamani dhidi ya wanne hao haukuzingatia vipengele hitajika na ushahidi huo haukuwa na uzito wa kuzuia makamishna hao kuapishwa.
Jaji Korir amefafanua zaidi uamuzi wake, akisema kwa sasa taifa linaelekea kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022 na kucheleweshwa kuapishwa kwa Makamishna hao huenda kukachangia taifa hili kushughudia mgogoro.
Itakumbukwa kwamba siku ya Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta aliwateua Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Abonyo kuwa makamishna wa IEBC na mapema leo wakaidhinishwa rasmi na bunge la kitaifa na kisha kuapishwa na Jaji mkuu nchini Martha Koome ili kuanza majukumu yao ya kikazi.