Familia zilizoathirika na mafuriko katika Kaunti ya Tana River zitanufaika na jumla ya magunia 1,500 ya chakula kuanzia juma lijalo.
Katibu Msimamizi wa wizara ya ugatuzi Hussein Dado amesema kamati maalum kutoka katika wizara hiyo inazuru kaunti ya Tana River sawia na kwengineko nchini kutathmini hali halisi ili kuwasaidia kwa mahitaji msingi waathiriwa hao.
Akizungumza mjini Hola, Dado amesema zaidi ya wakaazi 6,000 wamekatiziwa mawasiliano na usafiri kufuatia mafuriko yanayoendelea kuikumba kaunti hiyo akisema hali hiyo inaangaziwa vyema mno na serikali na wakaazi hao watasaidiwa.
Dado amehofia kwamba wakaazi hao watakumbwa na baa la njaa na hali ngumu kimaisha baada ya mimea yao kuharibiwa na mafuriko hayo na wanahitaji msaada wa dharura kutoka kwa Serikali.
Hata hivyo, Mbunge wa Garsen Ali Wario ameikosoa serikali kwa kuangazia maeneo mengine ya nchini yanayokabiliwa na mafuriko na kuisahau kabisa kaunti hiyo ya Tana River ambayo imeathirika zaidi na mafuriko hayo.